Sasa watumiaji wa iOS wanaweza kufunga WhatsApp kwa kutumia TouchID au FaceID

 

WhatsApp imekuwa ikija na mabadiliko na maboresho kadha wa kadha hasa upande wa usalama kwa miezi kadhaa sasa iliyopita. Moja ya maboresho waliyoleta kwa sasa ni ile ambayo ilikuwa ikiombwa sana na watumiaji. Kuanzia leo, watumiaji wa WhatsApp toleo la iOS wataweza kuongeza Touch ID na Face ID kama njia za nyongeza za usalama kufungua app hii.

Kutegemeana na simu ya iPhone, watumiaji wataweza kutumia kati ya Touch ID ama Face ID. Watumiaji wenye simu zilizo kwenye familia ya iPhone X watapata chaguo la Face ID, wakati wale wenye matoleo ya awali watapata chaguo la Touch ID. Simu zitakazofaidika na maboresho haya ni kuanzia iPhone 5s na kuendelea na zenye iOS 9 na zaidi. Kwa watumiaji ambao bado hawajaona mabadiliko watalazimika kusasisha app zao kupitia App store ili kupata toleo jipya kabisa ambalo ni 2.19.20.

Ili uweze kutumia huduma hii inabidi uende “Settings” –> “Account” –> “Privacy” kabla hujaweka “Screen Lock” on.

Japokuwa simu itaendelea kuonesha taarifa ya jumbe mpya za WhatsApp zinazoingia (kama umechagua message preview) hautaweza kusoma jumbe kwenye app mpaka simu ifunguliwe ambavyo inakuwa kwenye app zingine.

Inasemekana WhatsApp wanafanya majaribio ya sasisho kama hili kwa toleo la Android japo mpaka sasa hakuna taarifa zozote ni lini litaachiwa.

WAWEZA SOMA:  Project Linda: Kifaa kinachoibadilisha Simu yako ya Razer Phone kuwa Laptop

Andika Maoni

Andika maoni yako
Andika jina lako hapa