Kampuni ya Starlink inayotoa huduma za intaneti kupitia satelite, yenye makao makuu yake makuu huko Hawthorne, California, inatarajiwa kuanza kutoa huduma za intaneti nchini Tanzania kuanzia robo ya kwanza ya mwaka 2023, huduma hii ya intaneti ya kasi inatarajiwa kuongeza kasi ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Bilionea Elon Musk ambaye ndiye mmiliki wa Starlink, Tesla, SpaceX na sasa mmiliki wa Twitter, kupitia tovuti ya Starlink amesema amevutiwa na mazingira ya uwekezaji Tanzania na kampuni yake ya Starlink itafanya uwekezaji mkubwa kuanzia Mwaka 2023 endapo atapata kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari amethibitisha kuwa kampuni hiyo ya Starlink ilituma maombi ya kutoa huduma ya intaneti nchini kupitia tovuti ya TCRA.
SpaceX ambayo ni kampuni mama Ilianzishwa mwaka 2002 na bilionea Elon Musk kwa lengo lililoelezwa la kupunguza gharama za usafiri wa anga za juu ili kuwezesha watu kufika Sayari ya Mars.
Kampuni hii ambayo inajinadi kutoa intaneti ya kasi duniani kote, mpaka kufikia Juni 2022 imeripoti kuwa ina wateja zaidi ya 500,000 katika nchi 40. Mpaka sasa mataifa pekee ya Afrika ambayo yameanza kupata huduma za intaneti kutoka Starlink ni Nigeria na Msumbiji.
Hali ya upatikanaji wa Intaneti nchini Tanzania
Kwa mujibu wa ripoti ya robo ya nne ya mwaka 2021 kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), takwimu zinaonesha kuwa Watumiaji wa intaneti nchini Tanzania ni takribani milioni 29.8 ambao ni ongezeko la asilimia 4.4 kutoka idadi ya Watanzania milioni 28.5 kwa mujibu wa takwimu za robo ya mwisho ya mwaka 2020.
Zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanapata huduma ya intaneti kupitia simu zao za mkononi, na ingawa bei za data za simu za mkononi ziko chini (ukilinganisha na nchi zingine), bado hazijapatikana kwa bei nafuu kwa makundi ya watu ambao wengi wao wanaishi vijijini, na kusababisha pengo kubwa la matumizi ya intaneti kati ya mijini na vijijini.