Serikali ya Tanzania imetenga shilingi bilioni 45 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Anwani za Makazi Kuinua Uchumi wa Kidijitali. Mpango huu unahusisha kusimika miundombinu ya anwani za makazi na postikodi, mbawa, nguzo na vibao vya namba za nyumba katika halmashauri 194 zilizopo Tanzania Bara na Visiwani.
Amezungumza hayo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania Dkt Ashatu Kijaji akiwa mkoani Mwanza katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa uwekaji wa anuani za makazi katika nyumba mbalimbali pamoja na usimikaji wa nguzo zenye vibao vya majina kwenye Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambapo pamechaguliwa kama eneo la mfano ili kujifunza kwa lengo la kufanikisha utekelezaji huo ili kuzifikia halmashauri zote 194 nchini ambapo halmashauri 184 ni za Tanzania Bara na halmashauri kumi ni za Tanzania Visiwani
Lengo ni kuhakikisha kuwa kila mtaa unakuwa na jina lake na kila nyumba iwe na namba yake, hii inarahisisha utendaji kazi wa Serikali hata ndani ya jamii kwenye shughuli zetu za kiuchumi, tunaongelea kuwa na uchumi wa kidijitali, uchumi wa kidijitali hauwezekani bila kuwa tumekamilisha mfumo huu wa anwani za makazi -Dkt. Ashatu Kijaji
Mpaka muda huu ni jumla ya halmashauri 21 tu ambazo tayari zimefikiwa na kuanza kutumia mfumo huu wa huduma ya anwani za makazi, mfumo huu unarahisisha ufikishaji wa vifurushi katika maeneo ya kazi, ofisi na biashara.
Katibu Mkuu wizara hiyo, Dkt Zainab Chaula amesema awali utekelezaji wa mfumo huu ulifanyika nchi nzima lakini haukuwa na mafanikio na kuwa walichagua Jiji la Mwanza kama jiji la mfano, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 1.6 zimetumika kusimika miundombinu yote ya anwani za makazi, nguzo na vibao vya namba za nyumba katika mitaa yote 175 ya jiji la Mwanza.
Kazi ya utekelezaji wa anuani za makazi nchi nzima utatekelezwa na wananchi wenyewe waliopo kwenye maeneo hayo na itatoa fursa ya ajira kwa wananchi hao na ametoa rai kwa wananchi kuwa tayari kujitokeza kutekeleza mpango huo, kwani kwa sasa nguzo na vibao hivyo vinatengenezwa Jijini Dar es Salaam pekee na kusafirishwa kwenda mikoani kitendo ambacho hutumia gharama kubwa tofauti na vingetengezwa kwenye mkoa husika.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa wananchi wana kiu ya kujulikana kwa kuwa sasa mitaa yao ina majina na nyumba zao zina namba ambapo mwananchi analetewa mzigo wake pale alipo kwa kuwa sasa anatambulika mahali anapoishi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam wa Anuani za Makazi na Postikodi, Halmashauri ya Jiji la Mwanza ndugu Moses Seleki amesema kuwa jumla ya nyumba 108,000 zimefungwa namba za nyumba, nguzo 5,800 zimewekwa zenye vibao vya majina ya mitaa na nyumba 98,000 zimeingizwa kwenye mfumo wa anuani za makazi kwa simu ya mkononi.