App maarufu ya kutuma na kupokea meseji inayotumiwa na watu wengi zaidi duniani ya WhatsApp iko mbioni kuruhusu kutuma mafaili ya ukubwa wa 2GB. Kwa mujibu wa taarifa iliyopo kwenye tovuti ya WABetaInfo, mtandao huo uko mbioni kwenda sambamba na mpinzani wake Telegram, ambaye anatoa huduma ya kutuma mafaili makubwa ya mpaka 2GB tangu mwaka 2020.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa WhatsApp imeanza kufanyia majaribio maboresho hayo kwa idadi ndogo ya watumiaji wa iPhone. Watumiaji hawa ni wale wanaotumia toleo la majaribio na maboresho haya yameanza kuonekana katika toleo la majaribio la 22.7.0.76 la iOS. Maboresho haya yameonesha ongezeko la ukubwa wa mafaili yanayotumwa kupitia WhatsApp kufikia mpaka 2GB. Kwa sasa unaweza kutuma faili lenye ukubwa usiozidi 100MB kwa wakati mmoja.
Majaribio haya yanafanyika kwa watumiaji wa iOS nchini Argentina. Kupitia tovuti ya WABetaInfo imeambatanishwascreenshot kuwataarifu watumiaji kuwa sasa wanaweza kutuma mafaili makubwa, pia screenshot inaonesha kuwa kifaa kilichotumika ni kinachotumia mfumo endeshi wa iOS. Hata hivyo baadhi ya watumiaji wa toleo la majaribio kwa mfumo endeshi wa Android huko Argentina wameweza kuona mabadiliko haya.
Kwa sasa sisi tuliobaki tukae kwa kutulia kwani haijawekwa wazi ni lini watumiaji wengine wataweza kuanza kupata maboresho hayo kwa sababu inasemekana WhatsApp wana uwezo kurudisha ukubwa wa zamani baada ya haya majaribio.