Leo tarehe 16, Februari 2023 kampuni ya huduma za mawasiliano ya Airtel yawa ya kwanza kuzindua huduma ya kadi za eSIM Tanzania kwa wateja wake. eSIM (SIM iliyopachikwa) – ni mfumo wa kidijitali unaomuwezesha mtumiaji wa simu kupata huduma za mawasiliano bila kupachika laini kwenye simu. Unaweza kusoma zaidi kuhusu mfumo huu wa eSIM hapa.
Kupitia huduma hii, wateja wa Airtel wanaweza kusajili zaidi ya laini moja kwenye akaunti moja. Hii inamaanisha kwamba wateja wanaweza kuwa na simu mbili kwenye akaunti moja bila ya kuhitaji kadi ya SIM kwa kila simu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano alisema kuwa Airtel imefungua njia kwa kuwa mtoa huduma wa kwanza wa eSIM nchini Tanzania. Ameyasema haya leo jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya uzindduzi wa huduma hii,
Kulingana naye kampuni hiyo imekuwa ikiwekeza katika bidhaa na huduma za ubunifu zinazoendana na maisha ya kila siku ya kidijitali ya wateja wetu na uzinduzi wa eSIM ni ushuhuda wa dhamira yao kwa Tanzania.
Akifafanua zaidi, Bi. Singano aliongeza kusema kuwa huduma ya eSIM kwa sasa inapatikana kwenye mtandao wa Airtel na wateja wanaotaka kubadili kadi zao za sasa za SIM kwenda eSIM watahitaji kutembelea Duka lolote la Airtel nchini na kuongozwa kubadilishana SIM zao kwenda eSIM.
Wateja wanaweza pia kuongeza nambari mpya kwenye eSIM, wakati wanaendelea kutumia SIM za kawaida. Kwa kuwa na eSIM kutoka Airtel Tanzania, hawahitaji tena kuwa na simu kadhaa ili kubeba sim kadi na wanaweza kutumia hadi namba tano kwa simu moja.
Sio simu zote zinaweza kupata huduma hii ya eSIM. Kama wewe ni mteja wa Airtel Tanzania, unaweza kupiga *#06# ili kuona kama simu yako ina uwezo wa kutumia eSIM. Kuhusu kupiga *#06# kwa simu zinazooana namba ya EID itaonyeshwa’, akifafanua zaidi Singano amesema kuwa kadi ya eSIM haiwezi kuondolewa au kuibiwa, wakati kadi za SIM kawaida zinazoweza kutolewa wakati mwingine huibiwa, na kutumika katika utapeli hivyo usalama wa hali ya juu.
Msanii wa kizazi kipya, Diamond Platnumz ambaye alikuwepo kwenye uzinduzi wa huduma hii mpya na ya kwanza Tanzania, ameipongeza Airtel kwa kuzindua huduma hii nchini. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond ameonesha furaha yake kwa hatua hii ya kisasa na kuwahimiza wateja wa Airtel kuitumia huduma hii mpya.
Nini maoni yako kuhusu huduma hii mpya kutoka Airtel Tanzania? Tujulishe kwenye comment section hapo chini.