- Kuanzia teknolojia ya ugunduzi wa offside kwa kutumia AI hadi msaada kwa mashabiki wasioona, hapa tunakuletea kila teknolojia itakayotumika kwenye Kombe la Dunia la FIFA linaloendeshwa na teknolojia Qatar 2022.
Kadri teknolojia inavyozidi kukua ndio matumizi yanazidi kuongezeka. Matumizi ya Teknolojia kwenye michezo sio jambo ambalo limeanza hivi karibuni, hasa kwenye mchezo wa soka ama mpira wa miguu. Katika makombe kadhaa ya dunia yaliyotangulia tumeona teknolojia kadhaa mpya zikitumika katika kusaidia katika maamuzi uwanjani.
Mwaka 2010, wakati Qatar ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la 2022, ilianza kuandaa Dira ya 2020-23 ikijikita zaidi kwenye nia ya FIFA kutumia teknolojia katika soka.
Wazo ni kuongeza aina tofauti za teknolojia ili kuboresha uzoefu wa mchezo kwa mashabiki ndani na nje ya uwanja. Baadhi ya teknolojia hizi ni pamoja na AI au akili za bandia kusaidia kugundua offside, teknolojia ya kusaidia kwa mashabiki wasioona, teknolojia ya kudhibiti hali ya joto ndani ya uwanja, na mpira wenyewe una sensor za kugundua kasi ya mchezo.
Ungana nami nikikuangazia machache ya kiteknolojia ambayo unahitaji kuyafahamu katika Kombe la Dunia la Qatar 2022:
Teknolojia ya hali ya juu ya kupoza uwanja
Hali ya hewa ya joto kali na hali ngumu ya mazingira ya Qatar ndio kitu cha kwanza FIFA ilitaka kukabiliana nacho kwanza. Ili kuendana na hili, viwanja saba kati ya nane vinavyoandaa Kombe la Dunia la Qatar 2022 vitakuwa na teknolojia ya hali ya juu ya baridi ili kuweka hali ya hewa ndani ya uwanja baridi. Kituo cha nishati karibu na uwanja kitakuwa na uwezo wa kusukuma maji ya baridi katika bomba lililounganishwa na uwanja, ambalo lingebadilishwa kuwa hewa baridi na kusukumwa kwenye uwanja wa kucheza na maeneo ya kukaa watazamaji.
AI Rihla: Mpira rasmi wa Kombe la Dunia
Mpira huu ni wa 14 katika mfululizo wa mipira yenye teknolojia ya kisasa iliyotengenezwa na Adida kwa ajili ya mashindano makubwa ya mpira. Mpira huu una sensor ndani yake ambayo inaweza kugundua kasi na uelekeo wa mchezo. FIFA imedai kuwa mpira husafiri kwa kasi zaidi kuliko mpira wowote katika historia ya mashindano hayo.
Kwa kuongezea, mfumo wa suspension wa Adidas utasaidia kugundua eneo mpira ulipoguswa kwa usahihi mkubwa. Ubunifu wa mpira Al Rihla, ambayo inamaanisha ‘safari’ kwa Kiarabu, umeongozwa na utamaduni, usanifu, boti za kifahari, na bendera ya Qatar. Teknolojia ya offside pia ina kipengele cha kugundua matukio ya offside kwa sensor ya inertial measurement unit (IMU) iliyowekwa ndani ya mpira. Data ya mpira itatumwa kwenye chumba cha operesheni ya video zaidi ya mara 500 kwa sekunde.
Teknolojia ya kuotea (Semi-automated offside technology)
FIFA imetumia mfumo mpya wa kuchunguza msimamo wa soka na kuwasaidia waamuzi kufanya maamuzi sahihi, ya haraka na ya papo kwa papo wakati wa mashindano hayo Kwa msaada wa kamera 12 za kufuatilia kuzunguka uwanja na mpira wa Al Rihla, teknolojia hiyo itatoa tahadhari ya moja kwa moja kwa Mwamuzi Msaidizi wa Video kila wakati mpira unapochezwa kwa mchezaji katika nafasi ya kuotea. Hii itapunguza utegemezi wa marudio ya muda mrefu ya VAR ili kuamua kama mchezaji ameotea au la.
Teknolojia ya msaada kwa mashabiki wasioona
FIFA kwa kushirikiana na Bonocle and Feelix kuja na teknolojia itakayowasaidia mashabiki wasioweza kuona. Kampuni yenye makao makuu yake Doha ilianzishwa mwaka 2014 na Abdelrazek Aly and Ramy Soliman. Kwa kutumia teknolojia yao ya usaidizi kwenye changamoto za kuona wataweza kufurahi mashindano ya kome la dunia kama wengine.
Programu ya Mchezaji wa FIFA
Programu ya Mchezaji wa FIFA iliyotengenezwa na FIFA kwa kushirikiana na FIFPRO itatumika kwa mara ya kwanza nchini Qatar 2022. Programu hii itasaidia kutoa taarifa mbalimbali kuhusu mchezaji mmoja mmoja ikiwemo kasi, amegusa mpira mara ngapi, ameotea, amepiga pasi kwa usahihi kwa asilimia ngapi na mengine mengi.