Kampuni ya huduma za taxi ya Uber yasitisha huduma Tanzania. Uber ambayo hutoa huduma zake jijini Dar es Salaam imetoa taarifa hiyo ya kusimamisha huduma zake leo.
Kupitia chapisho kwenye tovuti ya Uber, wameandika sababu kubwa ya wao kusitisha huduma Tanzania ni changamoto ya nauli elekezi iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutoendana na gharama za uendeshaji wa huduma.
Nauli elekezi iliyowekwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesababisha changamoto kubwa kwa mifumo kama Uber kuendelea kutoa huduma kwa wateja wetu. Inakua ngumu kwetu kuendelea kutoa huduma.
Uber ambayo imekuwa ikitoa huduma za taxi kupita app yao tangu mwaka 2016 jijini Dar es Salaam wameandika Huduma zitasimamishwa rasmi kuanzia tarehe Tarehe 14 Aprili 2022.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, huduma zinazositishwa na Uber nchini Tanzania ni UberX, UberXL na UberX Saver. Usitishaji huu ni wa muda tu mpaka pale mamlaka husika zitakapokuwa tayari kushirikiana na wadau wa usafirishaji kuboresha kanuni zitazo leta ustawi wa teknolojia katika usafirishaji wa abiria.
Wiki hii madereva wa huduma taxi za mtandaoni za Bolt na Uber waliandamana kwenda ofisi LATRA kuhusu bei za nauli ili iwasaidie kufanya kazi kwa faida, wadau wa sekta ya usafiri wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ili kuleta unafuu kwa wananchi kutokana na gharama za usafiri zinazotarajiwa kupanda.