Leo Mei 18,2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa, Serikali ya Tanzania kujenga satelaiti yake ambayo itaweza kusaidia wananchi kupata mawasiliano na habari kwa haraka katika ikiwemo kutambua utekelezaji unaofanywa na Serikali na mengine yanayoendelea nchini na ulimwenguni kote.
Ameyasema haya akiwa kwenye uzinduzi wa Mradi wa Minara ya Kurusha Matangazo ya Televisheni Ardhini (DTT) ya Kampuni ya Azam Media Limited ambao umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 50 za Kitanzania ambao utahakikisha kuwa na uhakika wa matangazo ya Televisheni nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo imefanyika katika Viwanja vya Azam Media Hub Jijini Dar es Salaam,Rais Samia amesema minara hiyo ambayo imezinduliwa itaifanya nchi kuwa ya kwanza katika teknolojia ya 5G ambayo itatupatia huduma kiganjani bila kuwa na line ya simu ambayo ni mageuzi makubwa nani jambo la kujivunia kama Taifa.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema dunia imepiga hatua kubwa ya maendeleo, hivyo kama nchi hatuna budi kujiendeleza katika teknolojia za kisasa zitakasaidia kuboresha maisha.
Novemba 10, 2022 Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo alisema Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwa na satelaiti na kwamba katika mwaka huu wa fedha imeanza kuandaa utaratibu wa awali utakaowezesha kuunda na kurusha satelaiti yake angani.
Alisema ili kuwezesha kufikia azma hiyo tayari imeunda andiko dhana na kuunda timu ya watalaamu watakaoshauri aina ya satelaiti itakayorushwa angani itakayoendana na mahitaji halisi ya nchi.
Kundo alisema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza programu ya kuunda na kurusha setelaiti angani.
“Ni matarajio kuwa timu hiyo itakamilisha kazi ya uchambuzi na kuwasilisha mapendekezo yake Serikalini kwa hatua za kimaamuzi ndani ya mwaka huu wa fedha,” alisema Kundo.
Kwa mujibu wa Kondo, hadi sasa Afrika ina takriban satelaiti 50, na kuanzia mwaka 2016 ni satelaiti 20 tu ambazo zimekuwa angani, na kati ya hizo, ni tisa tu ambazo zimetengenezwa na zina taswira ya Kiafarika.
Misri ilikuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kutuma satelaiti angani mwaka 1998 huku Kenya ikiwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki.
Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutafuta teknolojia mbadala ya minara ya simu na mawasiliano ambayo kwa sasa inaongezeka kwa kasi.
“Tatizo nililonalo kichwani mwangu ni moja nikamwambia waziri (Nape Nnauye) minara 700 na mipya, kuna minara ambayo ipo ndani ya nchi, kuna minara ya Azam Media inakwenda kujengwa, kuna wengine watakuja kujenga nikamuuliza waziri hakuna teknolojia ya kuchanganya yote haya kwa sababu nchi hii itajaa minara,” amesema Rais Samia.