Zikiwa zimebaki siku chache kabla kongamano hili kubwa kuanza, tuwekane sawa kwanza. MWC (kwa kirefu ni Mobile World Congress ) ni moja ya matukio makubwa kabisa kwenye dunia ya teknolojia. Kampuni mbalimbali kubwa na zinazochipukia huonesha vifaa mbalimbali kwa ajili ya watumiaji wa kawaida ikiwemo simu za mkononi, tableti, vifaa vinavovaliwa kama smartwatch na vingine vingi. Kongamano hili kubwa ambalo hufanyika kila mwaka huko Barcelona, Hispania huendeshwa na muungano wa GSM (GSMA).
Katika kongamano la mwaka jana (MWC2017) tulipata kujionea simu mpya zilizovuma kama Huawei P10, Sony Xperia XZ Premium na LG G6 bila kusahau vifaa vingine vingi.
Kongamano MWC 2018 hili linaanza lini?
Kongamano hili limepangwa kuanza tarehe 26 ya mwezi wa pili 2018 na kuendelea mpaka tarehe moja ya mwezi wa tatu 2018, hata hivyo matangazo makubwa na ya muhimu yatatangazwa tarehe 25 ya mwezi wa pili ambayo ndio siku ya uzinduzi wa simu ya Galaxy S9. Litafanyika kwenye jiji la Barcelona nchini Hispania ambapo hufanyika kila mwaka.
Tutegemee kuona nini?
Samsung
Kati ya simu zinazosubiriwa kwa hamu kubwa ni Samsung Galaxy S9 na Samsung Galaxy S9 Plus. Vitu vinavojulikana kuhusu simu hizi mbili ni tarehe ya uzinduzi ambayo itakuwa ni February 25, 2018. Ki muonekano Samsung Galaxy S9 itafanana sana mtangulizi wake Samsung Galaxy S8 ila wametia mkazo mkubwa katika kuboresha kamera ambayo inasemekana itabadili jinsi tunavopiga piga picha.
Pia zitakuwa na spika zilizoboreshwa zaidi, kutakuwa na mode ya super slow motion kwenye video, kutakuwa na emoji mfano wa Animoji kwenye simu za Apple, kutakuwa bezel iliyopunguzwa zaidi, bila kusahau betri iliyoboreshwa zaidi.
Galaxy S9 inatarajiwa kuwa na prosesa ya Snapdragon 845 ambayo ni toleo jipya kabisa kutoka Qualicomm. Fingerprint scanner itakuwa chini ya kamera, na iris scanner iliyoboreshwa zaidi, pia sehemu ya kuchomeka headphones itakuwepo kama kwa watangulizi wake.
Nokia
Nokia wakiwa chini ya utengenezwaji na kampuni ya HMD Global wamefanikiwa kurudi tena kwenye mchuano wa simu, hata hivo mwaka jana waliachia Nokia 8 ambayo haikuwa tishio kwa wapinzani wake.
Mwaka huu tunatarajia Nokia 9 itaachiwa katika kongamano hili. Na tetesi zinaonesha Nokia 9 itakuwa na kioo chenye inchi 5.5 na teknolojia ya QHD OLED, yenye uwezo kutopitisha maji na vumbi, bezel ndogo kabisa na kamera mbili mbele na nyuma, inakuja na prosesa ya Snapdragon 845 na RAM kati GB 4 na GB 8 kwa mujibu wa tetesi, na betri yenye uwezo mkubwa bila kusahau iris scanner. Mpaka sasa HMD Global hawajathibitisha uzinduzi wa Nokia 9.
Sony
Mwaka huu Sony inasemekana itazindua Xperia XZ Pro japo Sony wanajulikana kwa kuzindua vifaa vingi kwa mpigo. Tetesi zilizozagaa karibu mwezi mzima sasa zinadai simu hii inakuja na kioo chenye upana wa inchi 5.7 na teknolojia ya 4K kama wenzake nayo itakuwa na prosesa ya Snapdragon 845. Sony ambao simu zao zinajulikana kwa kamera matata tunatarajia simu hii iwe na kamera mbili nyuma.
BlackBerry
Blackberry ambayo kwa sasa iko chini ya usimamizi wa kampuni ya TCL ilifanya vizuri mwaka jana ilipozindua BlackBerry KEYOne ambayo ilikuwa na keypad isiyohamishika. Mwaka huu tunatarajia TCL kuzindua simu mbili mwaka huu japo hatuna uhakika kama zote zitazinduliwa kwenye kongamano hili.
TCL ambao pia ni watengenezaji wa simu za Alcatel wamethibitisha pia kuachilia simu tatu za Alcatel ambazo zitakuwa za gharama nafuu ambazo zimepewa majina ya Alcatel 5 series, the Alcatel 3 series, na the Alcatel 1 series.
HTC
HTC amabo wamethibitisha kuwepo kwenye kongamano la mwaka huu, hawajathibitisha wataonesha bidhaa gani mwaka huu, maana simu yao mpya HTC U12, ambayo inatarajiwa kutoka mwaka huu, ripoti zinasema itazinduliwa katika onesho lao wenyewe na itakuwa kati ya mwezi wa tatu au wa nne mwaka huu 2018.
LG
Ripoti zilizotoka hivi karibuni zinaonesha LG kwa mwaka huu hakuna simu yoyote itakayozinduliwa kwenye kongamano hili baada ya kubadili utaratibu wa kuzindua simu. LG wanatengeza upya simu ya G7 na inaweza isitoke mpaka mwezi nne na inaweza kutoka kwenye onesho watakaloandaa wenyewe.
Bado tunaweza watarajia LG kuwepo kwenye kongamano la mwaka huu labda wanaweza kuzindua smnartwatch.
Tufuatilie kwenye mitandao mbali mbali ili usipitwe na Habari, Uchambuzi naMakala mbali mbali ya mitanadoni na ya kiteknolojia kwenye Facebook, Twitter, Instagram, Google+ na Youtube, Pia usisite kutoa maoni yako hapo chini au tuandikie barua pepe kwa [email protected]