Facebook, WhatsApp, Instagram, na Messenger zapotea hewani

Mwandishi Alexander Nkwabi
Katika hali isiyo ya kawaida leo jumatatu tarehe 4, oktoba 2021 tovuti, app na huduma zingine za Facebook, WhatsApp, Instagram, na Messenger zapotea hewani. Mitandao hii mikubwa ya kijamii ambayo yote inamilikiwa na kampuni ya Facebook imetoweka kuanzia saa 12 jioni majira ya saa za afrika mashariki, ambapo watumiaji wengi duniani kote wamekumbwa na sintofahamu baada kushindwa kufikia huduma za mitandao hii.

Kwa mujibu wa tovuti ya DownDetector na taarifa kutoka ukurasa wa facebook twitter, tatizo hili limetokea saa kumi na mbili na dakika 44 (saa za afrika mashariki), na limewaathiri watumiaji dunia nzima. Kufikia saa moja jioni watumiaji zaidi ya 50,000 waliripoti kukumbwa na tatizo hili.

Mitandao yote mitatu ambayo ni mali ya Facebook, inaendeshwa kwa kutumia miundombinu ya pamoja ambapo huduma zingine zinazomilikiwa na Facebook kama vile Facebook Workplace na tovuti ya Oculus pia nazo zimepotea hewani.

Kupitia Twitter, Mkuu wa mawasiliano Facebook bwana Andy Stone aliandika kuwa wanaelewa kuwa kuna watu wanapata changamoto kufikia huduma za mitandao hiyo na wanalifanyia kazi hilo ili huduma ziendelee kama kawaida. Pia ujumbe unaofanana na huo umeandikwa kwenye kurasa za instagram na whatsapp hukohuko Twitter.

Hii sio mara ya kwanza kwa mitandao hii inayomilikiwa na Facebook kupotea hewani mwaka huu, imetokea mara kadhaa ambapo tukio kubwa lilitokea mwezi wa nne, na lingine lilitokea mwezi wa sita 2021 ambapo inawezekana ndio kubwa zaidi kutokea ambapo instagram ilipotea hewani kwa zaidi ya masaa 16

Waswahili wanasema kufa kufaana, mitandao mingine ya kijamii ikiwemo Telegram na Signal imewakaribisha watumiaji wapya kuhamia kwenye mitandao hiyo wakisisitiza hakuna kupotea potea kwa huduma.

Pia kumeibuka meme mbalimbali zenye kuhusiana na tukio hili la kupotea kwa mitandao hii ya kijamii.

Muendelezo
Facebook yarudi hewani, pamoja na mitandao mingine ikiwemo Instagram na whatsapp.

Imejulikana tatizo lililoikumba Facebook mpaka kupotea ni matatizo ya DNS kwenye seva zake, hata hivyo tatizo hilo limetatuliwa na tayari mitandao hiyo imeanza kupatikana ena.

Kutokana na kupotea huko, mtandao wa Twitter nao mara kadhaa umeonekana kupotea, hii inasemekana ni kwa sababu ya kuzidiwa watumiaji kwani kwa mujibu wa taarifa Twitter imepata watumiaji wengi kupita wakati wowote ambao wamefungua mtanado huo kwa wakati mmoja tangu Twitter kuanzishwa.

Mwandishi Alexander Nkwabi Mhariri
Mitandao ya Kijamii
Alex ni mhariri mwandamizi hapa Mtaawasaba.com, kwa kipindi kirefu amekuwa akivutiwa na mfumo endeshi wa Android na michezo ya kompyuta. Alex akiwa haandiki hapa Mtaawasaba basi hupendelea kupiga picha, kusafiri na kusoma vitabu.
Maoni yako

Trending on Mtaawasaba

Receive Mtaawasaba notifications Click ‘Receive,’ then ‘Allow’ when prompted. Dismiss Receive